UTAMAUSHI WA WANAFUNZI SHULENI KATIKA RIWAYA ZA KISWAHILI: KIDAGAA KIMEMWOZEA NA CHOZI LA HERI .

  • JACKLINE NJERI MURIMI
  • Edith Muthoni Mwangi Chuo Kikuu cha Mount Kenya

Abstract

Mnamo karne moja iliyopita,elimu ilitolewa na wazee waliokomaa kwenye mazingira yasiyokuwa rasmi mathalani chini ya miti. Wanafunzi na ‘walimu’ hawa walilazimika kuketi pamoja kulingana na jinsia yao. Hata hivyo, jinsi siku zilivyosonga ndivyo masuala ya elimu yalivyobadilika na ambapo elimu ilifanywa kuwa rasmi. Walimu walipaswa kupitishwa kwenye kozi ya ufundishaji, muda maalum wa kufundishwa ulitengwa na mahali maalum kujengwa kwa ajili ya wanafunzi hawa kukusanyika wakati uliotengwa. Mahali kulikojengwa baadaye kulipewa jina mpya la ‘shule’. Jinsi miaka ilivyosonga ndivyo elimu shuleni ilivyoanza kutiliwa maanani na kulazimu watoto kujiunga nayo kwa wingi. Hata hivyo, takwimu zinaonyesha kuwa mwishoni mwa karne ya ishirini na mwanzoni mwa karne ya ishirini na moja baadhi ya wanafunzi wanazidi kutamaushwa na elimu na hivyo kuiambaa. Je, tatizo liko wapi ?

Utafiti huu ulikusudia kuchanganua sababu za wanafunzi kutamaushwa na elimu shuleni kwa mujibu wa riwaya za KidagaaKimemwozea ya Ken Walibora na ChozilaHeri ya Assumpta Matei. Kwa minajili ya kuafikia kusudio la utafiti wake, utafiti uliongozwa na malengo mahususi ambayo ni ; kujadili sababu zinazochochea wanafunzi watamaushwe na elimu shuleni kwa mujibu wa riwaya teule na kisha kuchanganua njia mbadala zinazopendekezwa na waandishi kupunguza utamaushi wa elimu kwa wanafunzi shuleni kwa mujibu wa riwaya hizi teule.

 Ili kupata data ya utafiti huu, mtafiti alitalii maktaba ili kusoma kazi za fasihi za waandishi mbalimbali zilizoandikwa kuhusu mada ya elimu kwa jumla. Mtafiti alikuwa na lengo la kusaka vitabu, magazeti, majarida pamoja na tasnifu za watafiti mbalimbali. Vile vile, mtafiti alisakura mitandaoni ili kuboresha data yake kwa kuangazia kazi za wasomi tofauti duniani kuhusu suala hili muhimu la elimu na faida zake kwa jamii ya mwanadamu.

Utafiti huu uliongozwa na Nadharia ya Uhalisia na ambapo sifa zake zilitumika kushughulikia masuala halisi ya utamaushi wa elimu kwa wanafunzi shuleni jinsi inavyoshuhudiwa katika jamii ya leo kama ilivyoangaziwa kwenye vitabu teule.  Ukusanyaji wa data ulipofikia hatima yake, mbinu ya kimaelezo ilitumika ili kuchambua data jinsi ilivyo na kisha ikawasilishwa kwa lugha ya nadhari huku mtafiti akizingatia malengo aliyokusudia. Kuna Imani isiyoterereka kuwa baada ya utafiti huu kufikia hatima yake, data iliyozalishwa itarutubisha maarifa yaliyoasisiwa na waandishi waliotangulia kuhusu masuala ya elimu na jinsi wanafunzi wa karne ya leo wanavyozidi kuchoshwa na elimu na kukata tamaa siku baada ya siku.

Published
2024-10-13