MABADILIKO KATIKA UTAMBULISHO WA WAHUSIKA WA JINSIA YA KIKE KATIKA TAMTHILIA: MIFANO KUTOKANA NA TAMTHILIA YA MAMAEE NA BEMBEAYAMAISHA.

  • Njeru Karimi Stella Chuo Kikuu Cha Mount Kenya
  • Dkt. Rose Kawira Chuo Kikuu cha Mount Kenya.

Abstract

Utafiti huu ulilenga kuchunguza mabadiliko ya utambulisho wa wahusika wa kike katika tamthilia mbili zilizochaguliwa: Mama Ee (1987) ya Ari Katini Mwachofi na Bembea ya Maisha (2022) ya Timothy Arege. Utafiti ulizingatia jinsi utambulisho wa wahusika wa kike unavyojibadilisha kwa kuzingatia kipindi na jinsia ya waandishi wa tamthilia hizi. Pia, uliangazia sababu zinazochangia mabadiliko haya katika uwasilishaji wa wahusika wa kike, kwa kuzingatia mazingira ya uandishi na mitazamo ya waandishi husika. Ni wazi kuwa fasihi hupata malighafi yake kutoka kwa jamii. Ili kutimiza lengo hili, nadharia ya Ufeministi wa Kiafrika iliyoanzishwa na Steady (1981) ilitumika. Utafiti huu ni wa kimaelezo na ulifanyika maktabani. Sampuli ilichaguliwa kwa kutumia mbinu za kusudi kwani ililenga vitabu maalum vya tamthilia vinavyoonyesha mabadiliko katika utambulisho wa mwanamke. Baada ya data kukusanywa, ilichambuliwa kwa njia ya kimaelezo kulingana na mihimili ya nadharia ya Ufeministi wa Kiafrika pamoja na malengo ya utafiti huu ambayo ni; kuchanganua utambulisho wa kike kisanii katika tamthilia za waandishi hawa wawili, kuchunguza athari za mazingira katika utambulisho wa kike katika tamthilia teule, na kubainisha athari za mitazamo ya waandishi hawa katika usawiri. Sura ya kwanza niutangulizi wa utafiti, ambapo mada ya utafiti, umuhimu wa utafiti, sababu za kuchagua mada, upeo na mipaka ya utafiti huu zimeshughulikiwa Sura ya pili inayoshughulikiamapitio ya maandiko kuhusu mada na misingi ya kinadharia iliyoongoza utafiti huu imejadiliwa. Katika sura ya tatu, muundo wa utafiti, eneo la utafiti, idadilengwa, uteuzi wa sampuli, ukusanyajidata, uchanganuzi wa data na uwasilishaji wa matokeo na maadili ya utafiti zimeshughulikiwa. Sura ya nne ni uwasilishaji na uchanganuzi wa data. Ile ya mwisho ni matokeo na mapendekezo ya utafiti huu.

Published
2024-10-13