Mitindo Iliyotumiwa Kufanikisha Uwasilishaji wa Mashairi Teule katika Diwani ‘’Nachora kwa Maneno’’na ‘’ Mashairi ya Wanyama”

  • JACKLINE NJERI MURIMI
  • Katunda Charo James Chuo Kikuu cha Mount Kenya
Keywords: Mitindo, Mashairi Teule, Nachora kwa Maneno, Mashairi ya Wanyama

Abstract

Maudhui ni mkusanyiko wa ujumbe na mawazo tofauti yanayojitokeza katika shairi fulani. Haya ni mambo yanayojadiliwa katika shairi, na yanaweza kuwa na mawazo mbalimbali. Maudhui husaidia kuunda dhamira ya shairi hilo, ambapo dhamira inamaanisha lengo, madhumuni, au nia ya mwandishi wa shairi.Ndani ya fasihi ya watoto tunapata mashairi ya watoto. Diwani “Nachora kwa maneno ya Swaleh Mdoe na mashairi ya wanyama ya Ali Hassan Kauleni na Elvera Shabiha ni diwani za mashairi ya watoto zinazotumika kufunza lugha ya Kiswahili nchini Kenya. Fasihi ya watoto ina sifa maalum zinazoiweka wazi. Kulingana na Wamitila (2008), sifa hizi ni pamoja na matumizi ya michoro yenye mvuto na ubora, lugha rahisi inayoweza kueleweka na watoto, na uwepo wa fantasia. Mara nyingi, wahusika wakuu katika fasihi ya watoto ni watoto wenyewe, na simulizi hizi hufungamana na motifu ya safari na msuko. Pia, fasihi ya watoto ina muundo rahisi, si mrefu sana, na huzingatia saikolojia ya watoto. Sifa hizi zinatokana na umri wa hadhira inayolengwa. Wamitila (2008) anabainisha kwamba fasihi ya watoto inavyoathiriwa na mtazamo wa jamii kuhusu watoto, na itikadi hii inaathiri jinsi tunavyoteua kazi za fasihi na matarajio yetu kuhusu kazi hizo, ikiwa ni pamoja na uandishi, dhamira, wahusika, na mwelekeo wake. Fasihi ya watoto inajumuisha nyimbo, mashairi, methali, vitendawili, ngano, hadithi fupi, na riwaya.

Fasihi ya watoto husaidia kukuza matumizi ya lugha. Mtoto anaposoma shairi, hujifunza msamiati mpya anaoweza kutumia katika mawasiliano yake ya kila siku. Shabaha za fasihi ya watoto ni kumwezesha mtoto kuingiliana vyema na wanajamii wengine. Aidha, inamsaidia mtoto kuzijua na kuzitukuza amali, hivyo kumpa msingi bora wa kuwa na sifa kamili za utu.

Ushairi ni sehemu ya fasihi inayotumia mpangilio maalum wa lugha, picha, na mapigo yaliyokusudiwa ili kueleza maudhui. Vigezo vinavyotumika kuchambua na kuainisha ushairi ni umbo lake pamoja na matumizi ya lugha. Kulingana na Senkoro (1982), ushairi hutumia lugha ya mkato inayotoa maudhui kwa muhtasari na mara nyingi huficha maudhui haya ndani ya taswira na ishara. King’ei (2000) anasema kwamba ushairi ni sanaa inayotumia lugha ya muhtasari iliyochanganuliwa kwa njia ya kiufundi ili kufanikisha athari iliyokusudiwa. Ameonyesha kuwa miundo ya mashairi hubadilika kulingana na mpito wa wakati, na ndiyo sababu mashairi kama utenzi, takhmisa, hamziya, na tumbuizo yanayofungamana na maudhui hayaandikwi kwa wingi.

Kila kazi ya fasihi ya watoto ina maudhui. Maudhui ndio ujumbe uliolengwa na mshairi katika kila shairi. Maudhui ya mashairi ya watoto yana maudhui yanayorejelea ulimwengu wa mtoto. Kahigi (1995) na mulokozi (1995) wanasema dhana ya ushairi inastahili kuzingatia umbo la ndani yani maudhui ili ujumbe umfikie mlengwa na kumwathiri kwa namna iliyokusudiwa.

Wahusika katika fasihi ya watoto ni sehemu muhimu ya kazi hizo. Wengi huwa watoto au wanyama na hurejelea maisha yao. Huwa hodari au wenye mapungufu yenye mafunzo kwa watoto. Kulingana na Bakize (2014), kwa kuwahusisha watoto, mtunzi anawapa nafasi ya kujitazama wenyewe kimatendo na hivyo kujirekebisha pale wanapokosa. Kwa hivyo, ni muhimu kutathmini wahusika wa mashairi.

Kwa mujibu wa Ngugi (2009) watoto husoma ili waweze kupata kukuza kipawa cha lugha, kuimarisha ubunifu wao pamoja na kujiepusha na tabia hasi. Hivyo mtindo wa mwandishi huchangia mashairi ya watoto kuufikisha ujumbe kwa hadhira. Hivyo kunahaja kuchanganua mtindo wa uandishi wa mashairi. Kipengele cha lugha ni zana muhimu katika kufaulisha kazi ya sanaa hususan mashairi ya watoto.

Author Biography

Katunda Charo James, Chuo Kikuu cha Mount Kenya

Mwanafunzi Idara ya Elimu Jamii, 

References

Coombes, H. (1991). Literature and Criticism. 160. Retrieved from https://books.google.com/books/about/Literature_and_Criticism.html?id=vJovAQAAIAAJ
Gituru, M. W. (2019). Unyambulishaji wa Vitenzi Katika Kigĩchũgũ (Doctoral dissertation, Chuka University).
Ismail, F. H. (2019). Kuchunguza Mtindo na Dhamira katika Tamthiliya ya Mondlane na Samora (Doctoral dissertation, The Open University of Tanzania).
Kimetto, H. K. (2016). Ulinganifu Wa Taarifa Za Habari: Tathmini Ya Tafsiri Kutoka Kiswahili Hadi Kikipsigis Katika Kituo Cha Kitwek (Doctoral dissertation, University of Nairobi).
Massoud, S. S. (2018). Kutathmini Matumizi ya Mtindo na Dhamira katika Tamthiliya za Mashetani na Mashetani Wamerudi: Utafiti Linganishi (Doctoral dissertation, The Open University of Tanzania).
Mwangi, P. K., & Munyao, J. K. (2016). Mtindo na Maudhui katika Nyimbo za Kisiasa za Msanii John De'Mathew nchini Kenya. Mulika Journal.
Nguti, M. (2013). Ulinganishi Wa Matumizi Ya Tasfida Za Muktadha Wa Nyumbani Katika Lugha Ya Kikamba Na Kiswahili (Doctoral dissertation).
Nyandiwa, H. (2015). Uchanganuzi Wa Kimtindo Wa Zinguo La Mzuka Na Mbaya Wetu (Doctoral dissertation, University of Nairobi).
Nyutu, J. (2016). Mtindo Katika Kazi Za Kubuni Za Leonard Sanja (Doctoral dissertation, University of Nairobi).
Stephano, R. (2022). Ukubalifu wa Tafsiri za Kitamaduni: Mfano wa Tafsiri ya Filamu ya Yesu kutoka Kiingereza kwenda Kinyaturu. Mulika Journal.
Tutaş, N. (2006). Critical thinking through literature. Ankara Üniversitesi Dil ve Tarih-Coğrafya Fakültesi Dergisi, 46(1), 93-108.
Wamitila, K. W. (2003). Kichocheo cha Fasihi: Simulizi na Andishi. 264. Retrieved from https://books.google.com/books/about/Kichocheo_cha_fasihi.html?id=6qcaAQAAIAAJ
Wamitila, K. W. (2008). Misingi ya Uchanganuzi wa Fasihi. Retrieved from http://erepository.uonbi.ac.ke/handle/11295/46826
Yunus, M. K. (2013). Masuala ya Kisiasa Katika Ushairi wa Kandoro: Mifano Kutoka Katika Mashairi Yake (Doctoral dissertation, The Open University of Tanzania).
Published
2024-10-15